8 Januari 2022 - 12:59
Baada ya makabiliano makali, Rais wa Kazakhstan atangaza kurejeshwa nidhamu, atoa amri ya kupigwa risasi “waasi”

Televisheni ya taifa ya Kazakhstan imemnukuu Rais wa nchi hiyo, Kassym-Jomart Tokayev, akisema leo Ijumaa kwamba nidhamu na utawala wa kikatiba umerejeshwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ni baada ya makabliano ya siku kadhaa yaliyopelekea kuuawa makumi ya watu kufuatia ghasia zilizoibuka kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta.

Rais wa Kazakhstan amesema - katika taarifa yake - kwamba "vikosi vya kurejesha utulivu vinafanya juhudi kubwa na utaratibu wa kikatiba umerejeshwa kwa kiasi kikubwa katika mikoa yote," akisisitiza kwamba operesheni za kurejesha utulivu zitaendelea hadi waasi hao watakapoangamizwa kikamilifu.

Rais wa Kazakhstan amesema katika hotuba yake ya leo Ijumaa kwa taifa kwa njia ya televisheni kwamba ameviamuru vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi waandamanaji bila ya onyo iwapo kutatokea fujo zaidi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kazakhstan imetangaza kuwa wahalifu 26 waliokuwa na silaha wameangamizwa na zaidi ya 3,000 wanazuiliwa, na kwamba polisi na askari 18 taifa wameuawa tangu kuanza kwa machafuko katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.

Russia imetuma "vikosi vya kulinda amani" nchini Kazakhstan kwa ombi la Rais Kassym-Jomart Tokayev wa nchi hiyo. Wanajeshi wa Russia waliwasili nchini humo jana Alhamisi.

Milio ya risasi ilikuwa ikiendelea kusikika mapema leo Ijumaa karibu na medani kuu ya jiji kubwa zaidi, Almaty, ambapo wanajeshi na waandamanaji walikabiliana vikali siku ya jana Alkhamisi.


342/